Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetangaza Operesheni Maalumu lengo ni kukomesha uhalifu ambao umeanza kurejea taratibu baada ya muda mrefu nchi kuwa katika hali ya amani na usalama.

Akizungumza  mbele ya Mkutano wa Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema kwa tathmini uhalifu umepungua sana nchini ila baadhi ya matukio machache yanayotokea yamekua yanapata mhemko mkubwa kutokana na njia za upashanaji habari kubadilika hivi sasa.

“Sisi kama Wizara kupitia Jeshi la Polisi tumejipanga, leo nimekaa kikao na IGP Sirro pamoja na Makamishna wake wote tumejadiliana kuimarisha hali ya ulinzi na usalama kwa wananchi wetu na sasa tunakuja na Operesheni ya Nguvu katika mikoa yote lakini la pili tunasisitiza ulinzi shirikishi maana Watanzania ni wengi ukizingatia idadi ya askari wetu,” amesema Simbachawene

Simbachawene ameiomba Wizara ya TAMISEMI kupitia Kamati za Ulinzi zinazoongozwa na Wakuu wa Mikoa na Wilaya hadi kushuka ngazi ya chini kushirikiana nao ili waweze kurudisha dhana ya ulinzi shirikishi ambayo itasaidia sana kukomesha uhalifu.

Akizungumzia tukio la mauaji ya mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 5 hadi 6 ambae mwili wake uliokotwa karibu na dimbwi la maji katika Kitongoji cha Usadala, Kijiji cha Utemini, Kata ya Ndono, Wilaya ya Uyui, Mkoa wa Tabora, Simbachawene amesema upelelezi wa awali unaonyesha kama alitupwa huku mwili ukiwa umeharibika sana, huku akiweka wazi uchunguzi wa jeshi la polisi unaendelea wakishirikiana na Mkemia Mkuu wa Serikali kubaini vinasaba vya mwili wa mtoto huyo kama alikuwa albino au la.

“Nimesikia baadhi ya taasisi za haki za binadamu wakinitaka niseme, nitoe kauli lakini nasema hapana maana upelelezi wa polisi una taratibu zake na tunaendelea kupeleleza kitaalamu juu ya tukio hilo, tunaomba watuamini ili tuache tufanye kazi kitaalamu” amesema Simbachawene

Akizungumza katika Mkutano huo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro amewataka wahalifu kuacha matendo ya hovyo mara moja huku akiweka nguvu ya jeshi katika kupambana na wahalifu.

“Ukitaka kuishi maisha mazuri na marefu acha uhalifu lakini kitendo cha kuendelea kufanya uhalifu ni kuichokoza serikali na niwaambie serikali ni ile ile,IGP ni yuleyule na Rais ni yule yule na ana madaraka ni yaleyale,watu watii sheria bila shuruti kuna watu wametoka gerezani wamerudia matendo yale yale waache hayo matukio kama wanapenda Watoto wao na familia zao” amesema IGP Sirro.

Watatu hatarini kuikosa Dodoma Jiji FC
Bodi ya mikopo kufuta tozo kwa wanufaika