Wizara ya Nishati, kupitia kwa Waziri wake Januari Makamba imetaja vipaumbele vya bajeti yake katika mwaka wa fedha 2023/2024 ikiwemo kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
Pia imepanga kupeleka umeme wa Gridi ya Taifa kwenye mikoa ya Katavi, Kigoma na Kagera na mradi mkubwa wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project) na imeanisha mambo yafuatayo.
A. Uzalishaji wa Umeme:
Kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme, ikiwemo kupeleka
umeme wa Gridi ya Taifa kwenye mikoa ya Katavi, Kigoma na Kagera na mradi mkubwa wa Kuimarisha Gridi ya Taifa (National Grid Stabilization Project).
- Uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika Gridi ya Taifa umeongezeka kwa asilimia 10.5 na kufikia MW 1,872.05 ikilinganishwa na MW 1,694.55 za mwaka 2021/22.
- Utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) – MW 2,115,
umefikia asilimia 86.89 ikilinganishwa na asilimia 60.22 za mwezi Aprili, 2022. - Hadi kufikia tarehe 23 Mei, 2023 kina cha maji ya Bwawa la JNHPP kilifikia mita 160.51 kutoka usawa wa bahari ambapo ili kuweza kuzalisha umeme, kiwango cha chini cha maji kinatakiwa kufikia mita 163 kutoka usawa wa bahari. Aidha, hadi kufikia tarehe hiyo, kiwango cha maji kilifikia mita za ujazo bilioni 11.8 sawa na asilimia 39.3 ya kiwango cha juu ambacho ni mita za ujazo bilioni 30.
- Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi I Extension – MW 185 umekamilika na kuchangia MW 185 katika Gridi ya Taifa. Utekelezaji wa mradi huo mwaka 2021/22 ulikuwa asilimia 88.
- Utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Rusumo – MW 80 umefikia asilimia 99 ikilinganishwa na asilimia 91.6 za mwaka 2021/22.
- Taratibu za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuzalisha umeme ya Kakono (MW 87) na Malagarasi (MW 49.5) zimekamilika.
- Miradi mingine ya kuzalisha umeme, ikiwemo kwa kutumia maji ya Ruhudji – MW 358, Kikonge – MW 321 na Rumakali – MW 222 na kwa kutumia Jua mkoani Shinyanga – MW 150 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.