Wizara ya  Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imesema kuwa imepokea kwa masikitiko makubwa ajali ya Lori iliyotokea eneo la Msamvu Mkoani Morogoro na kuwataka Watanzania wawe na moyo wa kusaidia badala ya kuhujumu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, ambapo amesema kuwa kumekuwa na tabia ya watu wengi kukimbilia kuchukua mali, badala ya kufikiria namna ya kumuokoa aliyepata ajali.

”Kwanza kabisa gari linapopata ajali, wito wetu kama Serikali, tunaomba Watanzania wawe kwenye moyo wakusaidia na sio kuhujumu, kwa muda mrefu baadhi ya Watanzania wenzetu ajali ikitokea, huwa wanakuwa kwenye hali yakutaka kuhujumu zaidi kuliko kuokoa, badala ya kufikiria kumuokoa mtu aliyepata ajali, huwa wanafikiria kumuibia badala ya kumuokoa hili ni jambo ambalo sisi kama Serikali tumeendelea kupambana kutoa elimu kwa Watanzania,” amesema Nditiye.

Aidha, Waziri Nditiye amesema kuwa, ajali iliyotokea leo ni matukio ambayo wananchi wengi wamekuwa wakikimbilia kuhujumu badala ya kumkimbilia dereva na utingo wake ili kuokoa maisha yao.

”Tunawaomba sana Watanzania tuache hiyo tabia, tujikite sana kuokoa mali na watu kila ajali inapotokea, tukijikita hivyo wala ajali kama hizi haziwezi kutokea na ni ajali ambayo imeua watu wengi sana” ameongeza Nditiye.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 11, 2019
Jeshi la Polisi latoa idadi kamili ya waliofariki kwenye ajali ya Lori Morogoro