Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja ameipongeza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kwa kazi nzuri ya usimamizi wa rasilimali za wanyamapori nchini, licha ya kuwa ni Taasisi changa kati ya zilizopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
Naibu Waziri huyo, ametoa pongezi hizo mara baada ya kutembelea ofisi za Makao Makuu ya TAWA zilizopo mkoani Morogoro, na kuzungumza na menejimenti na watumishi kuhusu masuala mbalimbali katika muendelezo wa ziara zake kwa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii.
“Pamoja na uchanga na uchache wenu kwenye Wizara mmeweza kushikamana vizuri, mmepokea majukumu yenu na mnafanya kazi nzuri usiku na mchana”, amesema Naibu Waziri.
Aidha, ameisisitiza mamlaka hiyo juu ya suala la anidhamu na uadilifu kwa watumishi wote na kuwataka wahifadhi kuzifuata na kuziishi kanuni za Jeshi la Uhifadhi.
Amesema, “Tufanye kazi kwa uadilifu tukiziangalia kanuni zetu za Jeshi la Uhifadhi, wale wachache wanaopaka madoa Jeshi letu tuwaepuke na ikiwezekana tuwaripoti.”
Katika ziara hiyo, Masanja ameiagiza TAWA kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu ikiwemo, zoezi endelevu la utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu namna bora ya kujilinda na wanyamapori wakali na kuongeza kasi ya ujenzi wa vituo vidogo vya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa TAWA, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi Mabula Misungwi Nyanda, amezungumzia masuala mbalimbali yakiwemo majukumu ya TAWA, mafanikio na changamoto mbalimbali zinazoikabili Mamlaka ikiwemo suala mtambuka linalohusu wanyamapori wakali na waharibifu.