Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inakusudia kuwa kitovu cha fursa katika Sekta ya TEHAMA Kitaifa na Kimataifa.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi ameyasema hayo wakati akifungua kikao Kazi cha uchambuzi wa fursa za kiuchumi za Sekta ya Mawasiliano kitaifa na kimataifa jijini Dodoma leo.
Amesema kusudi la kikao kazi hicho ni kuangazia fursa za kisekta zilizopo nchini na mchango wake katika kukuza uchumi wa nchi.
Dkt. Yonaz ameongeza kuwa, Serikali imelenga kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA ili waweze kutumia vyema fursa zinazokuwa zinajitokeza ndani na nje ya Tanzania.
“Serikali imeweza kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo watu pamoja na wadau ili kuhakikisha tunakuza sekta hii ya mawasiliano, kama mnavyo fahamu lazima tutekeleze mpango wa maendeleo kwa kuangalia yaliyomo ndani ya nchi yetu pamoja na mambo yanayoweza kuhamasisha,”alisema.
Aidha, amesema Wizara hiyo ina jukumu la kuchambua na kuangalia ni nchi zipi Tanzania inaweza kushirikiana nazo, lakini pia kuangazia suala la ujenzi wa minara na kuongeza uwezo wa kutumia simu janja pamoja na usalama wa mtandao.
“Tunatakiwa kuwa Wizara ya mfano kwa kupanua wigo wa fursa za kiuchumi na kuandika historia kwa kuifanya Sekta ya Mawasiliano kuchangia kwa kiwango kikubwa mabadiliko na mageuzi katika uchumi wa nchi yetu”, amesema Dkt. Yonazi
Kuhusu lengo la kikao hicho amesema ni cha kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kukuza uchumi kupitia TEHAMA sambamba na fursa zingine zilizo kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema amepokea maagizo ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, na watayajadili ili kuona ni mkakati gani utakaosaidia TEHAMA kuchangia pato la taifa kwa asilimia 3% ifikapo 2025.