Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, imelaani tukio la kuteswa kwa mtoto kwa kufungwa kamba mikono na miguu na kuning’inizwa, kisha taarifa hizo kurushwa kwenye mitandao ya kijamii.
Wizara imebainisha kuwa watoto wana haki ya kulindwa, kupendwa, kuendelezwa, kushirikishwa na haki zingine zote za binadamu na kwamba kitendo hicho ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa kifungu cha 13(1-3) cha sheria ya mtoto sura ya 13 ambapo adhabu yake ni kufungo kisichozidi miezi sita (6) au faini isiyozidi shilingi milioni tano au vyote viwili.
Tayari Jeshi la Polisi Tanzania limetangaza kumsaka mtu aliyemfanyia vitendo vya kikatili mtoto huyo mdogo kufatia video iliyokuwa inasambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mtoto huyo akiwa amefungwa kamba na kuning’inizwa kwenye nguzo za miti za uzio wa Mabati.