Wizara ya Fedha na Mipango ya Maendeleo nchini Liberia imepiga marufuku wafanyakazi wa kike wa wizara hiyo kuvaa wigi au kuweka dawa kwenye nywele zao.
Hatua hiyo imetokana na uamuzi wa wizara hiyo kuanza kutekeleza sera ya mwaka 2014 iliyoandaliwa na Serikali, inayopiga marufuku mawigi kwa watumishi wa kike.
Uamuzi huo umepingwa vikali na wafanyakazi wa kike ambao wamekaririwa na BBC wakidai kuwa ni unyanyasaji na ubaguzi wa kijinsia dhidi yao kuwaamulia mavazi na urembo.
“Hiyo sera ya Wizara ya Fedha na Mipango ya Maendeleo ni yakibaguzi. Rangi ya nywele ya mwanamke inaathiri vipi utendaji kazi wa kutimiza malengo ya wizara?” mtumishi mmoja amekaririwa.
Wengine wameielezea sera hiyo kuwa inatokana na mfumo dume ambao unataka kupanga namna wanawake wanapaswa kuonekana ingawa muonekano huo hauathiri utendaji wao wa kazi.
Sera hiyo ilitungwa wakati wa utawala wa Ellen Johnson Sirleaf, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo na baadaye kumkabidhi kijiti cha uongozi, George Weah.
Wigi na aina nyingine za nywele za wanawake zinazoagizwa nje hulipishwa kodi kwa mujibu wa sheria ya nchi hiyo.