Kundi kubwa la Vijana na Wanafunzi limo kwenye hatari ya kukumbwa na uhalifu wa mtandaoni kutokana na matumizi ya mitandao ya kijamii ya utafiti wa masomo na manunuzi ya kimtandao, kitu ambacho kimeifanya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita wapatao 250 wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Jangwani jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Stephen Wangwe amesema wanafunzi hao wanapaswa kuwa makini kabla ya kuchapisha jambo lolote ili kujikinga na uhalifu kama vile udhalilishaji, utapeli na udukuzi wa taarifa binafsi.

Elimu ya matumizi salama ya mtandao, ikitolewa kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Jangwani.

Aidha, Mhandisi Wangwe ameongeza kuwa elimu ya usalama mtandao ni muhimu sana ili watumiaji wa mitandao waweze kujilinda na athari zinazokuja na kukua kwa teknolojia ambapo wahalifu na wadukuzi nao hutumia teknolojia hiyo hiyo kufanya uhalifu na kugusa maisha ya watumiaji kwa kuharibu taswira na dira ya maisha yao.

Kwa upande wake, Mtaalamu wa Masuala ya Usalama Mtandao na Uchunguzi wa Kidijiti wa African ICT Alliance (AfICTA) kutoka Tanzania, Yusuph Kileo amewataka wanafunzi na vijana kutumia mitandao kwa uadilifu na kuzingatia usiri wa taarifa binafsi na kuhakikisha namba za siri za akaunti zao kutotabirika kirahisi.

Awali, Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani, Salum Kilipamwambu alisema licha ya somo ya TEHAMA kufundishwa shuleni hapo, bado kuna umuhimu kwa wanafunzi hao kujengewa uelewa kuhusu matumizi salama ya mtandao na kuwashukuru wataalamu wa Wizara kwa mafunzo hayo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, mwanafunzi wa kidato cha sita, Anna Ngowi amesema elimu ya usalama mtandao imewapa majibu ya nini cha kufanya, ili kujilinda na uhalifu mtandaoni na kuahidi watakuwa mabalozi wazuri kwa wanafunzi na vijana wenzao nchini.

Udhibiti wa mipaka kusaidia mapambano ya Ebola
OWMS 'yakimbiza' uendeshaji mashauri ya madai na usuluhishi