Mwanzilishi kitengo cha usalama wa Chakula cha Rais, Mzee Abdallah Chasamba (96) ambaye alikuwa ni kati ya waanzilishi wa Kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa – JKT, Ruvu baada ya uhuru mwaka 1961 amesema wizi uliowahi kufanywa na Vijana wa kuiba pesa za Pensheni za Wastaafu ambao ni marehemu, ulisababisha wengi wa walio hai kufutiwa malipo yao, wakihisiwa kufariki.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 Media nyumbani kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mzee Chasamba amesema anaushukuru uongozi wa Hayati Benjamin William Mkapa, kwa kuwaongezea kiasi kidogo cha pensheni hiyo, ingawa iliwasumbua kuipata kutokana na sababu hizo za wizi huku akishauri mamlaka husika kufanya tathmini ya mara kwa mara kuwatambua, badala ya kuhisi.
Amesema, “mara pensheni ikasitishwa na ikabidi nifuatilie kufika kule wanasema Mzee sisi tulidhani umeshakufa maana Vijana wetu hawa walikuwa wanaiba pesa za wazee waliofariki tukazifunga, nikawaambia mimi bado nipo hai na mngeuliza hata hapo Ikulu mngeambiwa mimi bado sijafa na ninashukuru bado nazipata.”
Hata hivyo Mzee Chasamba ambaye alikuwa Mkaguzi wa Chakula cha Rais Ikulu katika utawala wa awamu ya Kwanza amesema, alichanganyikiwa sana kusikia taarifa za kifo cha Mwalimu Nyerere kwani ni Kiongozi ambaye alifanya naye kazi kwa muda mrefu na kusema kila nafsi itaonja mauti, hivyo alimshukuru MUNGU na kumuombea apumzike kwa amani.