Meneja wa FC Barcelona Xavier Hernández Creus, amesema hakuna mchezaji aliyekataa kujiunga na klabu hiyo tangu alipokabidhiwa jukumu la kuwa mkuu wa Benchi la Ufundi huko Camp Nou.
Xavi alitangazwa kuwa Meneja wa klabu hiyo Novemba 06/2021, akichukua nafasi ya Ronald Koeman aliyeshindwa kufanya makubwa klabuni hapo, tofauti na alivyotarajiwa kabla ya kuajiriwa.
Meneja huyo ambaye aliwahi kuitumikia FC Barcelona kama Mchezaji na Nahodha kati ya mwaka 1998–2015, ametoa kauli hiyo, baada ya kuulizwa kuhusu kikao chake alichofanya na Mshambuliaji kutoka nchini Norway na klabu ya Borussia Dortmund, Erling Braut Haaland.
“Ni uthibitisho au swali? Angalia, mara zote ni vizuri kusajiliwa na Barcelona, kwangu, hii ndio klabu bora duniani, na kiukweli, hakuna hata mchezaji moja ambaye amesema hapana kwa Barcelona tangu niwe hapa kama Meneja.”
Alipoulizwa ni jinsi gani anawashawishi kuwasajili wachezaji, Xavi aliongezea, “Unawaelezea jinsi tunavyocheza na tunavyowafundisha, unawaambia watakugusa mpira mara 40 kwenye mchezo badala ya mara 20.”
“Najaribu kuwaacha waijue kuhusu klabu ni jinsi gani jiji lilivyo zuri. Naibadilisha hiyo kuwa nafasi ya dhahabu kwa mchezaji yeyote na aina ya uchezaji ambayo itawafanya wawe bora.”