Xavi Hernandez, alitaja uchezaji wa Barcelona dhidi ya Real Sociedad kuwa haukubaliki na akalaumu matokeo ya El Clasico licha ya kushinda bao 1-0 juzi Jumamosi (Novemba 04) kwenye Uwanja wa Reale Arena.
Ronald Araujo alifunga kwa kichwa bao pekee la ushindi dakika ya 92 na kubeba alama tatu baada ya mechi iliyokuwa imetawaliwa kwa sehemu kubwa na wenyeji.
Xavi alikiri kwamba Sociedad walistahili zaidi kwa uchezaji wao na alikosoa uchezaji wa timu yake, akisema wachezaji bado walikuwa wamelewa na kichapo cha mabao 2-1 juma lililopita kutoka kwa Real Madrid.
“Dakika 25 za kwanza hazikubaliki,” alisema kocha huyo wa Barca katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya mchezo.
“Ni kinyume na juma lililopita, tulipocheza vizuri na tulistahili kushinda, lakini tukashindwa. Juzi ni siku ya kujikosoa sana.
” La Real ni timu nzuri na walionesha nguvu zaidi kuliko sisi. Hatukuwa na raha hata kidogo. Tulikuwa na ‘hangover’ kutoka El Clasico. Tuliathiriwa zaidi na matokeo hayo kuliko nilivyofikiria.”
“Wakati wa mapumziko, niliwauliza wachezaji kama walikuwa wamechoka na wakaniambia hawakuwa wamechoka,” aliongeza Xavi.
“Kwa hivyo, niliwaambia wanapaswa kucheza kwa nguvu zaidi. Ilikuwa rahisi kama hivyo.
“Kipindi cha pili tulikuwa bora zaidi. Sare haitoshi kamwe. Tulifanya mabadiliko ya kushambulia na kushinda mchezo na kumaliza kwa nguvu.
“Tulikuwa vizuri katika dakika 10 za mwisho. Timu ilijisikia vizuri zaidi na tukatengeneza nafasi, Gavi akikaribia na kisha Ronald kupata bao.