Imefahamika kuwa Mshambuliaji wa zamani wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Yacouba Songne yupo mbioni kurejea nchini, huku klabu ya Geita Gold ikihusihwa kumsajili.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Burkina Faso aliondoka nchini mwishoni mwa msimu akiitumikia Ihefu FC na kutimkia Arta Solar7 ya Djibouti.
Geita Gold FC inahusishwa kuwa mbioni kumsajili Yacouba kupitia Dirisha Dogo la Usajili litakalofunguliwa juma lijalo.
Taarifa zilizothibitishwa na pande zote mbili zinasema, Geita inayosaka washambuliaji wawili wa kukiongezea nguvu kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu Bara na wameshaanza mazungumzo hayo na nyota huyo wa zamani wa Asante Kotoko ya Ghana.
Yacouba anayeitumikia Arta Solar7 ya Djibouti anataka kuondoka nchini humo baada ya kuona soka la nchi hiyo ni laini likikosa ushindani mkubwa kama ambavyo alitegemea huku akiwa kwenye kiwango kizuri tu tangu atue nchini humo ameshafunga mabao manane.
Geita imemvamia Yacouba haraka na mabosi wa klabu hiyo wakianza naye mazungumzo kwa siri ili waboreshe safu yao ya ushambuliaji ambayo imekuwa ikikosa makali kwenye mechi zao za ligi msimu huu.
Tulishaongea na kocha na alimpitisha unajua huyu ni mchezaji anayeijua ligi ya hapa na ameonyesha kiwango sahihi ngoja tuone tutafikia wapi naye,” amefichua mmoja wa mabosi wa juu wa klabu hiyo, huku Yacouba, amekithibitisha kuwa, ni kweli anazungumza na klabu hiyo, japo bado hawajafikia mwisho.
“Ni kweli Geita, imenitafuta kuna kiongozi wao tunaendelea kuzungumza, ila muafaka bado.”