Ziara ya Kitaifa aliyofanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini India, ililenga kuendeleza ushirikiano ambao tayari upo baina ya nchi hizi mbili hasa katika sekta za Afya, Viwanda, Biashara, Ulinzi na Usalama, Elimu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Uchumi wa Buluu, Maji na Kilimo.
Kwa mujibu taarifa iliyoandaliwa na Idara ya Habari – MAELEZO, imeeleza kuwa lengo lingine la ziara hiyo, ilikuwa ni kutangaza furIsa za Biashara na uwekezaji za Tanzania, ili kuvutia uwekezaji zaidi ambapo pia Viongozi mataifa hayo mawili walijadili kuhusu kushirikiana kulinda Wanyama hasa wa jamii ya paka ikiwemo chui.
Aidha, mazungumzo baina ya Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi yalilenga kupandisha hadhi ya mahusiano baina ya nchi hizi mbili waliouita “Ushirika wa Kimkakati”.
Nchi ya India imeonesha nia ya kutoa mafunzo kwa Wahandisi hasa wa masuala ya madini, usalama na ulinzi wa majini, biashara na uwekezaji, kujengeana uwezo, elimu na teknolojia hasa usalama wa mitandao na namna ya kushirikisha vijana kwenye masuala ya teknolojia.