Wakati Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba SC, Iman Kajula akiweka wazi kuwa wamejipanga vizuri kuhakikisha wanafanya maboresho makubwa ndani ya kikosi cha timu hiyo kuelekea michuano ya Africa Super League itakayoshirikisha timu kubwa nane barani humu, milango tayari ipo wazi kumnasa beki wa kushoto wa Ihefu FC, Yahya Mbegu.
Simba SC ni klabu pekee kutoka Ukanda wa Afrika Mashariki, itakayoshiriki michuano hiyo mikubwa Afrika ambayo inatarajiwa kuanza Oktoba mwaka huu.
Na kuelekea msimu mpya, Simba SC imekuwa ikihusishwa na usajili wa Mbegu, ambaye amekuwa katika kiwango bora zaidi msimu huu akiwa na kikosi cha Ihefu FC, na sasa mkataba wake unafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu na bado hajaanza mazungumzo ya kuongeza kandarasi nyingine na timu yake hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa Beki huyo tayari ameingia katika rada za Simba na yupo katika rada za viongozi wa Simba kwa ajili ya kuinasa huduma yake kwa msimu ujao.
Mtendaji Mkuu wa Ihefu FC, Zagalu Chalamila, amesema hawana taarifa au ofa kutoka Klabu ya Simba SC kuhitaji huduma ya Mbegu ambaye mkataba wake unafikia ukingoni baada ya ligi kumalizika.
Amesema nyota huyo yuko katika mipango ya benchi lao la ufundi akiwa miongoni mwa wachezaji ambao wamependekezwa na kocha kusalia ndani ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao.
“Mbegu mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu, bado hatujaanza kufanya mazungumzo na beki huyo, hatuna haraka naye, kama itatokea timu inamhitaji yeye ndiye ataangalia,” amesema Chalamila