Hukumu ya kesi dhidi ya aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wanne iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kujulikana leo, yaahirishwa tena hadi Desemba 11, 2019.
Kesi hiyo inayosimamiwa na Hakimu mkazi Mkuu, Janeth Mtenga imeahirishwa leo kwa mara ya tatu baada ya Hakimu kuomba muda wa kupitia jalada la hukumu.
Hukumu hiyo ilishagonga mwamba kutolewa takribani mara mbili kutokana na sababu tofauti ikiwemo ya Hakimu aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo kuhamishwa Kituo cha kazi, kesi hiyo ilikuwa na mashtaka 30 lakini ilipofikia katika uamuzi wa kama washtakiwa wana kesi ya kujibu ama laah! walipunguziwa mashtaka 10 na kubakiwa na mashitaka 20.
Washtakiwa wengine waliobakia katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Katibu wa shirikisho hilo, Selestine Mwesigwa na Karani wa TFF, Flora Rauya, wanakabiliwa na mashtaka mbalimbali yakiwamo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa Dola za Marekani 173,335.