Kiungo Kinda wa Barcelona, Lamine Yamal anatazamiwa kuzuia nia za timu za Ligi Kuu England kusaka saini yake msimu ujao kwa kusaini mkataba mpya wenye kipengele chenye masharti magumu.

Kinda huyo machachari mwenye umri wa miaka 15 ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuichezea Barcelona baada ya kuingia akitokea benchi katika ushindi ilioupata Aprili mwaka huu dhidi ya Real Betis.

Pia, Yamal aliweka rekodi kuwa mfungaji bora kinda zaidi wa timu ya taifa ya Hispania kuwahi kufunga alipofikisha umri wa miaka l6 akifunga katika ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya Georgia katika mechi ya kimataifa.

Kuongezeka kwa kasi ya kijana huyo kulimfanya aingie kwenye orodha fupi ya timu kadhaa za Ligi Kuu England ambazo zinawania saini yake ikiwemo Manchester City.

Kwa mujibu taarifa Yamal yupo tayari kuongeza mkataba mrefu wa kuendelea kuichezea Barcelona kwa mujibu wa mkali wa masuala ya usajili Ulaya, Fabrizio Romano.

Inaaminika kwamba kinda huyo atasaini mkataba mrefu wenye kipengele chenye thamani ya Pauni Bilioni Moja kwa klabu zinazomtaka.

Kocha Xavi Hernandez ana nia ya kuhakikisha kuwa Yamal haendi popote kufuatia kiwango bora alichoonyesha katika mechi tisa alizocheza.

Licha ya umri wake mdogo, Yamal anaweza kuwa na uwezo wa kumrithi Lionel Messi ambaye anakipiga Inter Miami ya Marekani kwa sasa.

Lakini yeye sio kinda wa kwanza kuandaliwa mkataba mrefu wenye thamani ya Pauni Bilioni Moja, ila wapo makinda wengine kama Pedri, Gavi na Ansu Fati anayekipiga Brighton kwa mkopo.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Oktoba 3, 2023
Kocha Singida FG awatupia lawama wachezaji