Klabu za ligi kuu ya soka nchini England, zimekubaliana dirisha la usajili litalazimika kufungwa kabla ya kuanza kwa ligi hiyo, kuanzia msimu ujao.

Mjadala huo ambao uliibuliwa na umoja wa mameneja wa klabu za ligi kuu nchini England, umefungwa rasmi hii leo kwa kupigiwa kura, na kura za ndio zilikua 14 dhidi ya 6 za hapana.

Maamuzi hayo tayari yameshapewa baraka na chama cha soka nchini England (FA), ambayo pia yatazinyima nafasi klabu za ndani kufanya uhamisho wa mchezo kutoka kwenye ligi za chini hadi ligi kuu, pamoja na nje ya nchi hiyo, baada ya ligi kuanza mwezi August tofauti na sasa.

Kwa mantiki hiyo msimu ujao wa 2018/19, dirisha la usajili kwa England litafungwa rasmi August 09.

Kwa kawaida dirisha la usajili nchini England lilikua likifungwa mwishoni mwa mwezi August ama mwanzoni mwa mwezi Septemba, lakini mameneja wa klabu za ligi kuu waliona mpango huo umekua ukiwaharibia mikakati yao hasa wanapoviandaa vikosi vyao kabla ya ligi kuanza (Pre-Season).

Hata hivyo dirisha la usajili wa majira ya kiangazi kwa nchi nyingi za barani Ulaya hufungwa inapofika August 31.

Kikwete, Zitto wanena makubwa kuhusu Lissu
Tabia za Rooney zaanza kumkera Koeman