Misaada yenye thamani ya shilingi milioni 5, imetolewa kwa kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu cha Tumaini Children centre kutoka kwa wanachama na Mashabiki wa Yanga mkoani Kagera katika sherehe za kusheherekea mafanikio ya timu yao msimu wa 2022/23.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Msemaji Mkuu wa mashabiki tawi la Yanga Mkoani Kagera Jamali Kalumna amesema lengo kubwa la kutoa mdaada huo ni kurejesha faraja kwa watoto hao na kumshukuru Mungu kutokana na kuwa na wakati mzuri msimu uliomalizika.

Mashabiki na wanachama wa Yanga Mkoa wa Kagera, wakicheza ngoma ya kihaya na watoto wanaolelewa kituo cha Tumaini Children Center.

Amesema, “wote tumekuja hapa kwa mapenzi makubwa kwaajili ya kutoa sadaka yetu kwa kumshukuru Mungu kwa mema, makubwa ambayo ameitendeka timu ya Yanga mwaka 2022/23 tunasema asante sana Mungu.”

Akitoa neno la shukrani, Mwalimu na Mlezi wa Kituo hicho kilichopo kata ya Kyakailabwa manispaa ya Bukoba, Hosea Mkebezi, ameeleza kuwa kituo hicho mpaka sasa kina uwezo wa kuhudumia watoto zaidi ya 61 ambao wanawapata kutoka mazingira tofauti tofauti ndani na nje ya manispaa ya Bukoba.

Msemaji Mkuu wa wanachama wa Yanga mkoa wa Kagera, Jamali Kalumna akitoa hamasa kwa watoto yatima na wanaoishi mazingira magumu kituo cha Tumaini Children Center.

Kwa upande wake mtoto anayelelewa kituoni hapo Letisia Abel amesema “tunashukuru kwa msaada ambao tumeupokea kutoka kwenu timu ya Yanga Mungu awabariki na awatangulie vitu hivi mlivyovitoa hasa chakula ni msaada mkubwa kwetu”.

Baadhi ya vitu vilivyotolewa na wanachama hao wa Yanga mkoa wa Kagera ni pamoja na sukari, nguo, mchele, viatu, juisi, chumvi, sabuni na kuwalipia kisimbuzi kwaajili ya kufatilia michezo ikiwemo mpira wa miguu.

Makabi Lilepo aomba kuvunja mkataba Al Hilal
Hii hapa tafsiri halisi ya neno Katerero