Magoli manne ya Azam FC dhidi ya Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Tanzania bara yameifanya iongoze kundi B kwa kufikisha pointi saba kombe la Mapinduzi huku ikimaliza mechi yake kwa kishindo cha magoli 4-0 kwenye uwanja wa Amaan visiwani,Zanzibar.
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC wafikishe jumla ya pointi saba baada ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja wakati Yanga wameshika nafasi ya pili wakiwana pointi 6 wakiwa wameshinda mbili na kufungwa moja.
Sasa Azam itacheza na mshindi wa pili wa Kundi A katika Nusu Fainali, wakati Yanga itacheza na mshindi wa kwanza wa kundi hilo na kuna uwezekana Yanga akakutana na Mahasimu wake wakubwa timu ya Simba.
Hadi mapumziko, Azam walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Nahodha , John Bocco, maarufu kama Adebayor aliyefunga goli la mapema dakika ya 1 baada ya shuti la Salum Abubakari kutemwa na Dida na kumkuta mfungaji akiwa katika sehemu nzuri.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko hata hivyo vijans wa kocha wa muda wa Azam FC Idd Nassor Cheche walifanikiwa kupata magoli matatu na kuwachanganya wachezaji wa Yanga pamoja na mashabiki huku wakiwa hawaamini kilichotokea.
Mshambuliaji Mghana, Yahya Mohammed alifunga bao la pili dakika ya 54 kwa kichwa akimzidi maarifa beki Andrew Vincent ‘Dante’ baada ya krosi ya Sure Boy.
Joseph Mahundi akafunga bao zuri zaidi kwenye mchezo huo dakika ya 80 kwa shuti la umbali wa mita zaidi ya 20 kuipatia Azam bao la tatu baada ya pasi ya Sure Boy.
Winga Mghana, Enock Atta Agyei aliyetokea benchi kipindi cha pili, akaifungia Azam bao la nne dakika ya 85 akimchambua vizuri kipa Dida baada ya pasi ya Samuel Afful aliyeingia kipindi cha pili pia.
Kwa ujumla vijana wa George Lwandamina walicheza chini ya kiwango na kucheza ovyo mno na Azam ingeweza kupata ushindi wa kihistoria kama ingetumia nafasi zaidi ilizotengeneza wangeshinda hata magoli kumi na kuendelea.