Uongozi wa klabu ya Yanga umemfuta kazi aliyekua kocha mkuu wa timu hiyo, Mwinyi Zahera kutokana na kile kilichoelezwa ni matokeo mabovu ya msimu huu ndani ya Ligi na michezo ya kimataifa.
Taarifa hizo zimethibitishwa leo na mwenyekiti wa timu hiyo Dkt Mshindo Msolla akiongea na waandishi wa habari ambapo nafasi yake imechukuliwa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa, Charlse Boniface Mkwasa atakayekaimu kwa muda wa wiki mbili kabla ya kumpata Kocha Mkuu.
Kwa upande wake msemaji wa timu hiyo, Antonio Nugaz kupitia akaunti yake ya instagram aliweka picha akiwa na Zahera huku akiambatanisha na maneno ya kuthibitisha kuachana na kocha huyo raia wa DR Congo.
”Ilikua vyema kufanya kazi na wewe Mwinyi Zahera na benchi lako zima la ufundi.. shukrani sana ‘see you again’.
”Rasmi club yetu imeachana na Mwalimu Mwinyi Zahera na benchi zima la ufundi na nafasi yake itakaimiwa na Charles Boniface Mkwasa,” alisema Nugaz.
Yanga imeachana na Zahera ambaye msimu uliopita aliongoza timu hiyo kucheza michezo 18 ya ligi kuu bara bila kufungwa mpaka ilipodondokea kufungwa na Stand United uwanja wa Kambarage kwa bao 1-0.