Nyota kutoka DR Congo Yannick Bangala amewataka Waamuzi wanaochezasha Ligi Kuu Tanzania Bara kuwa makini na kutoyafumbia macho matukio yanayofanywa kwa makusudi kwa lengo la kuwaumiza wengine.
Bangala anayemudu nafasi ya Beki wa Kati na Kiungo Mkabali, ametoa kaili hiyo baada ya kufanyiwa tukio la Rafu Mbaya akiwa katika mchezo wa Young Africans dhidi ya Coastal Union uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha juzi Jumamosi (Agosti 20).
Bangala amesema kitendo alichofanyiwa kilikua cha wazi na alitarajia kuona Mwamuzi anatoa adhabu lakini haikuwa hivyo na badala yake mambo yaliendelea kama kawaida.
Amesema Waamuzi wanapaswa kufahamu Wachezaji wengi wamekua wakiutumia mchezo wa Soka kama ajira inayoendesha maisha yao, hivyo hawana budi kuwalinda kwa kuwakanya wachache wenye makusudi ya kuwaumiza wengine wanapokuwa Uwanjani.
“Nimefanyiwa tukio baya sana katika mchezo wa juzi, nikiri nilichofanyiwa hakikuwa sahihi katika mchezo wa soka, nilitarajia Mwamuzi huenda angetoa adhabu kwa mchezaji aliyenifanyia vile lakini haikuwa hivyo, watu wafahamu kuwa mchezo wa Soka ni Burudani sio Vita, tusikie hatua ya kutaka kuumizana na kuharibiana Karia zetu.”
“Tukio nililofanyiwa kila mtu ameliona na sio mara ya kwanza kufanyiwa ukatili kama huo mimi sio muongeaji ni mtendaji uwanjani kwa kucheza, lakini imefikia mahali natakiwa kujitetea ili nisikilizwe kilio changu nahitaji kucheza mpira kwa sababu ndio ajira yangu.” amesema Bangala
Katika mchezo huo Young Africans iliibuka na ushindi wa 2-0 mabao yakifungwa na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison na Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele.