Aliyekua kiungo wa klabu bingwa nchini England Manchester City Yaya Toure amejiunga na klabu yake ya zamani ya Olympiakos, inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Ugiriki.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 35, ambaye aliwahi kuitumikia FC Barcelona ya Hispania kwa mafanikio makubwa, amerejea kwenye klabu hiyo, baada ya kufikia makubaliano binafsi na uongozi wa klabu hiyo, huku akiwa mchezaji huru.

Kabla ya kufanya maamuzi ya kurejea nchini Ugiriki, Toure alikua anahusishwa na taarifa za kujiunga na moja ya klabu za jijini London, hasa baada ya wakala wake Dimitri Seluk, kuwasilisha taarifa hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter juma lililopita.

Toure aliihama Olympiakos mwishoni mwa msimu wa 2005-2006 na kuelekea FC Barcelona na baadae Man City.

“Nilipoondoka hapa mwaka 2006, niliahidi nitarudi, nimetimiza ahadi, nimerudi rasmi,” Ameeleza kiungo huyo wa Ivory Coast kupitia tovuti yake.

“Nimefanyua maamuzi haya kutokana na mapenzi ya dhati na klabu hii, uhusiano wetu ulikua unaendelea tangu nilipoondoka, ninaamini marafiki wawili ni vigumu kuachana zaidi ya kutenganishwa na kifo.”

Klabu ya Olympiakos inayoongoza msimamo wa ligi ya nchini Ugiriki mpaka sasa haijatoa taarifa rasmi za makubaliano waliyofikia na kiungo huyo, japo baadhi ya vyombo vya habari nchini humo vimeeleza kuwa, Toure atakua akipokea mshahara wa Euro milioni 2.5 sawa na Pauni milioni 2.25 kwa mwaka.

Msimu uliopita klabu hiyo ilimaliza katika nafasi ya tatu, ikiwa ni mara yao ya kwanza ndani ya miaka 23, huku wakichagizwa na rekodi ya kutwaa ubingwa wa Ugiriki mara 20 katika miaka 22 iliyopita.

Ronaldo de Lima kuimiliki Real Valladolid
Serikali ya Libya yatangaza hali hatari