Kiungo Mshambuliaji wa Manchester City, raia wa Ivory Coast, Yaya Toure ameeleza kusikitishwa kwake na kutoshinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika wa mwaka iliyoenda kwa Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon.

Toure ameeleza kuwa kitendo cha yeye kuikosa tuzo hiyo ni aibu kubwa kwa Afrika kwa sababu alikuwa na vigezo vyote vya kuendelea kuichukua tuzo hiyo aliyoibeba miaka mitatu iliyopita.

Akiongea katika mahojiano maalum na RFI, Toure alionesha jinsi alivyosononeka moyoni kwa kile alichokiita Afrika kutothamini vitu vyake.

Hivi ndivyo alivyoeleza:

“Nimekatishwa sana tamaa. Inasikitisha kuona Afrika inajibu hivi, kwamba hawafikirii mafanikio ya Afrika ni muhimu.  Nadhani hii ndiyo inayoiletea Afrika aibu, kwa sababu kufanya hivyo sio sawa. Lakini sasa sisi tufanyeje kuhusu hilo? Sisi waafrika, hatuoneshi kwamba Afrika ni muhimu katika macho yetu. Tunatukuza zaidi kilicho nje zaidi ya bara letu wenyewe. Hii inasikitisha,” alisema Yaya Toure.

“Nimekuwa nikiambiwa mara nyingi, huwezi kuitunza Afrika kupita kiasi kwa sababu Afrika itakuwa ya kwanza kukuangusha,” alisisitiza na kuongeza kuwa hata FIFA pamoja na kuwa na historia mbaya ya rushwa isingeweza kufanya uamuzi kama uliofanywa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Mchezaji huyo alitoa mfano kuwa yeye kuwa mchezaji pekee wa Afrika aliyetajwa kwenye orodha ya kuwania tuzo ya Ballon d’Or kati ya wachezaji 23 ilionesha dhahiri kuwa ndiye anayestahili kushinda tuzo ya mchezaji bora wa Afrika.

Hata hivyo, Yaya Toure pia aliponda uamuzi wa FIFA  kumtaja yeye peke yake kutoka Afrika kwenye orodha ya wachezaji 23 wanaowania Ballon d’Or  akidai kuwa hawakutenda haki kwa Afrika.

TFF Yatoa Shukuran Kwa Watanzania Waliompokea Samatta
Picha: Bilionea Wa Unga 'El Chapo' aliyetoroka Gerezani Akamatwa tena