Maafande wa Polisi Tanzania wamemsajili beki mkongwe Kelvin Yondani aliyeachwa na Young Africans mwishoni mwa msimu uliopita, baada ya kumaliza mkataba na kushindwa kuongeza mwingine kutokana na kushindwana kimaslai.
Yondani alilazimika kukaa pembeni pasina na kucheza soka kwenye klabu yoyote kwa kipindi cha nusu msimu, hivyo kusajiliwa na maafande hao wa Jeshi la Polisi, kutamfanya aonekane tena katika viwanja vya soka nchini.
Taarifa zilizothibitishwa kutoka ndani ya uongozi wa Polisi Tanzania Zimeeleza kuwa, pande hizo mbili zimekubaliana kusaini mkataba wa miezi sita, huku uzoefu wa Yondani ukitarajiwa kusaidia kuongeza nguvu ndani ya kikosi.
“Ni kweli tumemalizana nae na ataanza kuitumikia klabu yetu muda wowote kuanzia sasa akisaidiana na Iddy Moby na Mohamed Kassim kuhakikisha timu yetu inakuwa imara kwenye safu ya ulinzi,” kilisema chanzo hicho huku kikisisitiza kuwa usajili huo ni pendekezo la mwalimu.
“Walinzi waliopo hawana tatizo ni imara lakini mwalimu ameona kuna umuhimu wa kuongeza nguvu na ameangalia ubora wa Yondani ikiwa ni sambamba na uzoefu wake anaamini atawasaidia wachezaji waliopo,” alisema.
Awali ilielezwa kuwa, Yondani huenda angeibukia kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAF) Namungo FC, lakini taarifa za kumalizana na Polisi Tanzania zinamaliza uvumi huo.