Nahodha wa zamani na beki wa Young Africans, Kelvin Yondani huenda akasaini mkataba mpya na uongozi wa klabu hiyo, kufuatia mkataba wake wa sasa kuwa ukingoni.

Mkataba wa beki huyo aliyedumu kwa muda wa miaka minane tangu alipoikacha Simba SC, utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu wa 2019/20.

Yondani ambaye kwa sasa ndio mchezaji mkongwe ndani ya kikosi cha Young Africans, huenda akasaini mkataba wa mwaka mmoja, Kutokana na umri wake kuendelea kumtupa mkono, kwani hana muda mrefu sana wa kuendelea kusakata kabumbu.

Mpango wa kusaini mkataba mpya kwa beki huyo ambaye pia ni muhimili wa kutumainiwa kwenye kikosi cha Taifa Stars, umechagizwa msimamo wa mabosi wa klabu hiyo kongwe ambao wanahitaji kumuona Yondani akistaafu kwa heshima.

Imeelezwa kuwa tayari kocha mkuu Luc Eymael alikuwa amependekeza asakwe mbadala wa Yondani, na ndipo msimamo huo wa viongozi ulipojitokeza.

Pamoja na kuwa mmoja wa mabeki bora kuwahi kutokea nchini Tanzania, Yondani alikubali kucheza Young Africans hata katika zile nyakati ngumu ambazo wachezaji wazuri walikuwa wakikimbilia timu nyingine.

Baada ya Nadir Haroub kustaafu kwa heshima Young Africans, Yondani atapewa nafasi hiyo pale atakapoamua kustaafu.

Mbunge mmoja atajwa kupata maambukizi ya Corona Tanzania
Newcastle United kuweka rekodi mpya England