Aliyewahi kuwa Beki wa Simba SC ambaye kwa sasa anakipiga Geita Gold, Kelvin Yondani ameipongeza Klabu hiyo ya Msimbazi licha ya kuondolewa tena kwenye hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya tatu na moja Kombe la Shirikisho.

Simba SC Ijumaa (Aprili 28) iliondolewa kwenye hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa ugenini kwa mikwaju ya Penati 4-3 dhidi ya Wydad AC ya Morocco baada ya matokeo ya jumla ya bao 1-1, Simba SC ikishinda bao moja Uwanja wa nyumbani na kukubali kipigo kama hicho ugenini.

Yondani ambaye alisajiliwa Young Africans akitokea Simba SC amesema kitendo cha kikosi cha Mnyama kuondolewa katika hatua ya Robo Fainai tena na Bingwa mtetezi, hakipaswi kubezwa bali kinapaswa kupongezwa.

Beki huyo amesema wachezaji wa Simba SC wanatakiwa kujipongeza kwa kuwa wanazidi kupiga hatua msimu hadi msimu pamoja na kushindwa kufikia lengo lao la kutinga hatua ya Nusu Fainali.

“Simba SC ndani ya misimu miwili nyuma walianza kwa kuruhusu mabao mengi ugenini.”

“Msimu huu wamefika Robo Fainali na kukutana na mabingwa watetezi kwenye taji hilo tofauti na matarajio ya wengi wanaweza kufungwa mabao mengi, wameondolewa kwa mikwaju ya penati,” amesema.

Yondani amesema uongozi na Benchi la Ufundi la Simba SC ni muda sahihi kwao kujifanyia tathimini ili kufahamu nini kinawakwamisha kufikia malengo yao huku akisisitiza anaiona kwenye hatua kubwa msimu ujao ambao tayari wamejihakikishia ushiriki.

Wakati huo huo, amesema kitendo cha watani zao Young Africans kutinga hatua ya Nusu Fainali kimewapa nguvu mpya Simba SC kutokata tamaa na kuongeza nguvu ili kuweza kufikia lengo na wao.

“Simba SC misimu minne wamefikia hatua hiyo huku Young Africans ukiwa ni msimu wao wa kwanza kufikia hatua ya Robo Fainali na kufuzu Nusu Fainali, naamini mafanikio hayo yatawapa wakati motisha watani zao,” amesema.

Kutinga kwa Simba SC Robo Fainali ni mara ya nne katika misimu mitano ya karibuni ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho na tatu za Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Serikali yapiga marufuku uhamisho holela
Kocha Namungo FC atamba kuibanjua Simba SC