Wakati kikosi cha Young Africans kikitarajiwa kushuka dimba la Uhuru kesho Ijumaa kuikabili JKT Tanzania kwenye mchezo wa ligi kuu, mabingwa hao wa kihistoria huenda wakawakosa nyota wao watatu Kelvin Yondani, Metacha Mnata na Abdulaziz Makame ambao walikuwa timu ya Taifa.
Stars imewasili leo alfajiri kutoka Tunisia ambako ilicheza mchezo wa kuwania kufuzu michuano ya Afcon 2021 na kufungwa mabao 2-1 na Libya.
Kaimu Kocha Mkuu wa Young Africans Charles Mkwasa huenda akachukua tahadhari ya kutowatumia wachezaji hao, kwani hawatakuwa wamepata muda wa kutosha kupumzika baada ya safari ndefu.
Nyota mwingine wa Young Africans aliyekuwa na majukumu ya timu ya Taifa ni Patrick Sibomana ‘PS’ ambaye alikuwa na timu ya Taifa ya Rwanda iliyocheza dhidi ya Cameroon Novemba 17 na kufungwa bao 1-0.
Wakatu huo huo, baada ya kuwa na mwanzo mzuri Young Africans, Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Mkwasa huenda akainoa timu hiyo mpaka mwishoni mwa msimu
Wakati akitangaza kuvunja benchi la ufundi mapema mwezi huu, Mwenyekiti wa Young Africans Dk Mshindo Msolla alisema Mkwasa angeiongoza Yanga katika muda wa mpito kabla ya kumpata kocha mpya.
Lakini tangu akabidhiwe majukumu hayo, timu imeonekana kubadilika jambo ambalo limewafanya mabosi wa Young Africans wasitishe kwa muda mchakato wa kusaka kocha mpya.
Mkwasa ameendelea na mipango ya kuimarisha timu ikiwa ni pamoja na kupendekeza maboresho yanayotakiwa kufanywa wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Hata hivyo matokeo mazuri ndio yatakayo-muhakikishia kupewa mkataba wa kudumu.