Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara imeendelea tena hii leo kwa mchezo mwingine wa kiporo kuchezwa jijini Dodoma kati ya Maafande wa Jeshi La Kujenga Taifa (JKT Tanzania) dhidi ya Young Africans kutoka jijini Dar es salaam.
Mchezo huo uliounguruma kwenye Uwanja wa Jamuhuri, umeshuhudia miamba hiyo ikipapatuana vilivyo ndani ya dakika 90, huku kila mmoja akizisaka alama tatu muhimu kwa udi na uvumba.
Mpaka kipyenga cha mwisho kinapulizwa Young Africans kutoka jijini Dar es salam walijikuta wakiambulia alama moja, baada ya kulazimisha sare ya bao moja kwa moja dhidi ya wenyeji wao JKT Tanzania.
Michael Aidan alitangulia kuipatia bao la kuongoza JKT Tanzania kwa kupiga shuti kali nje ya 18 na kufanikia kumtungua mlinda Mlango wa Young Africans Metacha Mnata dakika ya 36.
Young Afriucans walipata bao la kusawazisha dakika ya 76 kwa bao la Patrick Sibomana alieumalizia mpira uliokua umetemwa na mlinda mlango wa JKT Tanzania Aboubakar Barwany, baada ya kushindwa kuhimili shuti kali lilipigwa na kiungo Haruna Niyonzima.
Kwa matokeo hayo Young Africans wanafikisha alama 55 ambazo zinaendelea kuwaweka kwenye nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi kuu, huku JKT Tanzania wakifikisha alama 43 wakiwa nafasi ya saba.