Kikosi cha Young Africans kimerejea jijini Dar es salaam kikitokea Khartoum, Sudan kilipokwenda kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Hilal.
Young Africans ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa 1-0 na kutolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, huku Al Hilal ikitinga Hatua ya Makundi ya Michuano hiyo msimu huu 2022/23.
Rais wa klabu ya Young Africans Injinia Hersi Said amesema wamekubali matokeo na sasa wanajipanga kucheza mchezo wa mtoano wa Kombe la Shirikisho ili kusaka nafasi ya Kucheza Hatua ya Makundi ya Michuano hiyo.
Amesema kilichotokea ni kama wamefunguliwa dirisha lingine la Michuano ya Afrika, hivyo hawana budi kuanza kujiandaa na mchezo huo ambao mpinzani wake atafahamika kesho Jumanne (Oktoba 18) baada ya kufanyika Droo mjini Cairo, Misri.
“Tumekubali tumepoteza mchezo dhidi ya Al Hilal, haikuwa rahisi kucheza mchezo ule katika Uwanja wa Al Hilal, tulioyaona wakati wakicheza dhidi ya St George ya Ethiopia, jana ndio ilikua ‘Full Episode’, bado tupo kwenye Michuano ya Afrika, ni kama tumefungua dirisha lingine.”
“Mpinzani wetu tutamfahamu baada ya Droo ya kesho na mchezo wa kwanza naamini utachezwa kati ya Novemba 04-06, tutahakikisha tunapambana ili kuwa sehemu ya timu zitakazofuzu.” amesema Hersi Said
Young Africans imetolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya sare ya 1-1 kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, na jana ilifungwa 1-0 ugenini.