Uongozi wa Klabu ya Young Africans umesema mechi ya Jumamosi dhidi ya Al Ahly imeshikilia heshima yao kwani kama ikiibuka na ushindi itapata sifa kubwa barani Afrika na pia itarudisha matumaini yao na malengo ya kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu 2023/24.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kwa sasa wapo Unguja kwa ajili ya kupata baraka kutoka kwa wàzee, wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa ajili ya mechi ya Jumamosi (Desemba 02) itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

“Tuko Zanzibar kwa ajili ya kupata baraka, kuelekea katika mechi yetu dhidi ya Al Ahly, ni mchezo mkubwa ambao umeshikilia heshima yetu barani Afrika, ni mpinzani mkubwa, hivi karibuni anakwenda kucheza Klabu Bingwa Dunia, atakwenda kucheza na klabu kubwa barani Ulaya kama Manchester City na nyinginezo, maana yake huyu ni mpinzani sahihi kwetu na taiheshimisha klabu yetu kama tukipata matokeo mazuri,” amesema Kamwe.

Itakuwa ni mechi ya pili ya Young Africans kwenye Kundi D, baada ya ile ya awali iliyopita kupokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad nchini Algeria na inahitaji ushindi ili irudi kwenye reli ya kuelekea hatua ya Robo Fainali.

Al Ahly, ikiwa nyumbani Jumamosi (Novemba 25) nayo iliichakaza Medeama ya Ghana mabao 3-0.

Mabingwa hao watetezi, Al Ahly, wapo juu kileleni mwa msimamo wa Kundi hilo kialfabeti tu, wakiwa sawa kwa kila kitu na CR Belouizdad iliyo kwenye nafasi ya pili, huku Young Africans nayo ikiburuza mkia kialfabeti pia kwani iko sawa kila kitu na Medeama iliyokaa nafasi ya tatu.

Kevin de Bruyne kurudi Man City 2024
Kagere atoa ufafanuzi ushangiliaji wake