​​​​​​​Wakati Mashabiki, Wanachama na Viongozi wa Simba SC wakijivunia juhudi zao za kuiwezesha Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwa msimu ujao, Klabu ya Young Africans imesema itashiriki michuano hiyo kwa msuli wao, na si kupitia nafasi zilizotengenezwa na watani wao hao wa jadi.

Young Africans wamekua wakisisitiza hilo, kwa kuamini endapo watashiriki michuano ya kimataifa msimu ujao kupitia juhudi zilizofanywa na Simba SC, itakua kama aibu kwao.

Mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Young Africans Injinia Hersi Said amesema wamejipanga kuiwezesha timu yao kumaliza katika nafasi nzuri upande wa Ligi Kuu na michuano ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ ili kupata nafasi ya kuwakilisha nchi kimataifa.

“Hatuiandai Young Africans kwa kuiangalii Simba, hatutegemei pia mtu kucheza michuano ya CAF, haijalishi wametengeneza nafasi ngapi, sisi tutaifunga Biashara na kucheza fainali.

“Mshindi kati ya Simba na Azam FC tutamfunga fainali na kutwaa Kombe la FA na kwenda kucheza Kombe la Shirikisho Afrika bila kumtegemea mtu yeyote,” amesema Hersi

Aidha, amesema pia anajivunia mambo makubwa ambayo Young Africans imefanikiwa kwa msimu huu 2020/21, ikiwamo kutwaa Kombe la Mapinduzi, baada ya kuifunga Simba SC kwa changamoto ya mikwaju ya Penati, mjini Unguja visiwani Zanzibar mapema mwaka huu.

Young Africans inatarajiwa kucheza Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Biashara United Mara mjini Tabora kwenye uwanja wa Ally Hassan Mwinyi, huku Simba SC ikijipanga kukutana dhidi ya Azam FC mjini Songea mkoani Ruvuma, katika Uwanja wa Majimaji mwishoni mwa mwezi huu,

Upande wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans iliyocheza michezo 29, inashika nafasi ya pili ikiwa na alama 61, huku Simba SC iliyocheza michezo 27 ikiendelea kuongoza msimamo wa Ligi hiyo kwa kufikisha alama 67, na Azam FC iliyocheza michezo 30, ipo nashika nafasi ya tatu ikiwa na alama zake 60.

Huu ndio mkakati wa kuchochea Uchumi shindani - Mwigulu
Kova awajibu Mashabiki, Wanachama Simba SC