Uongozi wa Young Africans umeapa kumpigania Fiston Kalala Mayele ili asiondoke mwishoni mwa msimu huu, kwa lengo la kuendelea kuwa na kikosi bora chenye safu imara ya ushambuliaji.
Kauli hiyo ya Young Africans imekuja, kufuatia tetesi kudai kuwa, Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika RS Berkane wanajiandaa kuwasilisha ofa ya kumsajili Mshambuliaji huyo aliyetupia mabao 14 katika Ligi Kuu Tanzania hadi sasa.
Mayele alijiunga na Young Africans mwanzoni mwa msimu huu akitokea AS Vita ya DR Congo, ambapo ameonesha kiwango kikubwa cha kufunga mabao akiongoza kwa ufungaji Ligi Kuu Bara akiwa nayo 14 sawa na George Mpole wa Geita Gold.
Makamu Mwenyekiti wa Young Africans, Frederick Mwakalebela, amesema ni ngumu kwao kukubali kumuachia mshambuliaji aina ya Mayele, hivyo wapo tayari kutumia kiwango chochote cha fedha ili wafanikishe malengo yao ya kumbakisha.
Ameongeza kuwa, kikubwa watakachokifanya ni kuboresha baadhi ya mahitaji yake atakayoyataka ili asiondoke kikosini kwao.
“Tunafahamu umuhimu mkubwa wa michuano ya kimataifa, kama yalivyokuwa malengo yetu ni kufika nusu fainali kimataifa, hivyo ni lazima tuwe na kikosi imara kitakachotufikisha huko.
“Hivyo hatutakubali kumuachia mchezaji yeyote muhimu na tegemeo katika timu yetu kuelekea msimu ujao ambao tunaamini ndio utakuwa wenye mafanikio kwetu.
“Hivyo hao Berkane watafute mchezaji mwingine, lakini sio Young Africans, kwani hatutakubali kumuachia mchezaji yeyote muhimu akiwemo Mayele na wengine,” amesema Mwakalebela.