Mwenyekiti wa klabu ya Young Afrcans Dkt. Mshindo Msolla amesema uongozi wa timu hiyo umemaliza tofauti iliyojitokeza na wadhamini wao kampuni ya GSM.
Akizungumza mapema leo katika Mkutano wa pamoja na GSM, Dk Msolla amesema GSM wataendelea na majukumu yao kama ilivyokuwa mwanzo “Tunatambua na kuthamini mchango ambao wenzetu GSM wamekuwa wakitoa kwa klabu yetu.
“Baada ya changamoto iliyojitokeza siku chache zilizopita, sisi kama uongozi wa Young Africans tulichukua hatua kwa mujibu wa taratibu zetu na baadae tuliomba kukutana na wenzetu GSM”
“Nashukuru kikao chetu killikwenda vizuri na leo tunatangaza rasmi kuwa GSM wataendelea na majukumu yao. Wataendelea kutimiza wajibu wao kulingana na mkataba tulioingia nao. Lakini pia wataendelea kufanya yale waliyokuwa wakiyafanya ambayo sio sehemu ya mkataba,” alisema Dk Msolla.
Naye Mkurugenzi wa uwekezaji GSM Mhandisi Hersi Said amesema wao ni wanafamilia wa Young Africans hivyo wataendelea na yale yote waliyokuwa wakiyafanya lengo likiwa kuhakikisha wanaitoa klabu hiyo hapo ilipo.
Mhandisi Hersi amesema wataendelea kushirikiana na uongozi wa Yanga pamoja na Mwanayanga yeyote mwenye mapenzi mema na klabu hiyo.
Amesema sehemu kubwa ya kazi wanayoifanya kwa Young Africans wanajitolea kwa sababu wanaipenda, huku akiwakaribisha wadau wengine ambao wangependa kuiona inasonga mbele waungane nao.
Katika hatua nyingine Hersi ametanabaisha kuwa, baada ya kukosa ubingwa kwa misimu mitatu, amewataka wanayanga kuweka malengo ya kutwaa ubingwa msimu ujao.
Amesema Young Africans inatarajiwa kuwa na mabadiliko makubwa ikiwemo kusajili wachezaji wapya ambao wataweza kutimiza azma hiyo ya kushinda ubingwa msimu ujao “Hili nataka niliingie vichwani mwa Wanayanga wote. Baada ya kukosa ubingwa kwa misimu mitatu, msimu ujao ni zamu yetu kutwaa ubingwa.”
“Tunaanza mikakati mapema kwa kuboresha timu yetu ikiwemo kusajili wachezaji wenye uwezo na kuwatengenezea mazingira mazuri wachezaji ambao tutaendelea kubaki nao.”