Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umesema bado haujafahamu sababu za kutoalikwa kwenye Mkutano Mkuu wa Kawaida wa Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’, uliofanyika Jana Jumatano (Agosti 10).
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Young Africans Wakili Simon Patrick akizungumza na kituo cha radio cha E-FM Radio amesema wamelazimika kufuatilia mkutano huo kupitia mitandao baada ya kutopata mualiko.
Simon amesema Young Africans ambao ni Mabingwa wa nchi walitamani kuwepo katika mkutano huo unaonendelea jijini Arusha na kuhudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani ‘FIFA’.
“Bahati mbaya hatujajua kipi kimetokea na sisi (Yanga) kukosa mualiko, tuliamua kutumia fursa ya teknolojia tuweze kufuatilia mkutano huu,” amesema Simon.
“Ni jambo jema tunafurahi limerfanyika hapa Tanzania, kwa manufaa mapana ya nchi yetu wamepata kutangaza utalii, wamepata kujionea mazuri ya Tanzania.”
Aidha Simon ameongeza ingawa mkutano huo ni wa ‘CAF’ lakini wanafahamu kwamba Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ ndio walipaswa kutambua nafasi ya Young Africans kushiriki mkutano huo kwa kuwapa klabu yao mualiko.