Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wamejipanga kuibomoza Klabu ya Asec Mimomas, ikihusishwa na usajili wa wachezaji watatu kutoka katika timu hiyo ambao wote wamefanya vizuri msimu uliopita 2022/23.
Asec Mimosas ambao wanashiriki ligi kuu ya nchini Ivory Coast, kwa msimu uliopita walifanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi hiyo huku kwenye michuano ya kimataifa wakifika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Chanzo chetu cha ndani kutoka nchini Ivory Coast tayari kimeeleza kuwa kuwa, Young Africans wapo katika mipango ya kuibomoa timu hiyo huku wakihusishwa na usajili wa wachezaji watatu ambao ni beki wa kulia Yao Attohoula, kiungo wa kati Zoungrama Mohammed na winga Kramo Kouame Aubin.
“Ni kweli Young Africans wapo katika mazungumzo na baadhi ya wachezaji kutoka ndani ya ASEC Mimosas, kuna wachezaji watatu ambao Young Africans wapo katika mipango ya kuwasajili na sio lazima wawasili wote lakini kati ya hao kuna ambao watawasajili.
“Yupo namba sita Zaongram, beki wa kulia Yao na winga Aubin Kramo, hawa wote wapo katika mipango ya Young Africans japo siwezi kufahamu kama wote watasajiliwa lakini kikubwa ni kwamba wote mikataba yao na Asec Mimosas imemalizika jambo ambalo ni rahisi Young Africans kuwapata,” kimesema chanzo cha kuaminika.