Wawakilishi pekee waliosalia katika michuano ya kimataifa Young Africans, kesho asubihi wanatarajia kuondoka Dar es salaam kuelekea mjini Hawassa, Ethiopia kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili wa kuwania kufuzu hatua ya makundi ya kombe la shirikisho dhidi ya Wolaita Dicha.
Young Africans wataelekea nchini Ethiopia huku wakiwa na akiba ya ushindi mabao mawili kwa sifuri walioupata katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Dar es salaam, uwanja wa Taifa mwishoni mwa juma lililopita.
Kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa anatazamiwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi katika mpambano huo, kufuatia kuondoka kwa mkuu wake Geroge Lwandamina ambaye hakuonekana kazini tangu katikati ya juma hili.
Wasaidizi wengine wa benchi hilo ambao watakua katika msafara wa kesho ni Noel Mwandila (Mzambia) na Juma Pondamali.
Mchezo wa mkondo wa pili kati ya Young Africans dhidi ya Wolaita Dicha utachezwa jumatano, Uwanja wa Hawassa.