Wakati Kocha Mkuu wa Young Africans, akianika mikakati yake kuelekea mechi mbili za nyumbani za Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Medeama FC na CR Belouizdad, wachezaji wa timu hiyo wamesema nao wamepania kupambana hadi tone la mwisho la hatua hiyo ya Makundi.

Aidha, Gamondi amesema atatumia mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar kusaka pointi tatu pamoja na kuwapa mbinu wachezaji wake kwa ajili ya kuwinda alama sita zitakazofufua matumaini yao ya kucheza Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kikosi cha Young Africans kilireje nchini jana Jumapili (Desemba 10) tayari kujiandaa kwa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Jumamosi (Desemba 16) kabla ya Jumatano ya wiki ijayo (Desemba 20) kuikaribisha Medeama FC katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam kwenye mechi ya marudiano ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo uliopita, Young Africans ililazimisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Waghana hao, hivyo kufikisha pointi mbili, matokeo ambayo yanaifanya kuburuza mkia kwenye Kundi D, linaloongozwa na Al Ahly ya Misri ikiwa na alama tano ikifuatiwa na Medeama na Belouizdad ya Algeria ambazo kila moja ina pointi nne.

Kocha Gamondi amesema licha ya kuwapo kwa mchezo mgumu kutafuta alama tatu muhimu, lakini hawawezi kusahau mechi ya ligi dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo ni muhimu kushinda kwa ajili ya kufikia malengo yao mama kwa msimu huu.

Amesema anatambua umuhimu wa kila mchezo, baada ya mechi yao dhidi ya Medeama FC, wamerejea kujiandaa dhidi ya Mtibwa Sugar lakini wakitarajia kutumia mechi hiyo kama maandalizi ya mchezo huo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tunatambua tuna mechi mbili nyumbani na tunahitaji kuvuna alama zote sita, dhidi ya Medeama FC na CR Belouizdad, kabla ya mchezo huo tuna kibarua kigumu mbele yetu dhidi ya Mtibwa Sugar, tunatakiwa kushinda kabla ya kucheza michezo miwili ya kimataifa.

“Kabla ya kuanza kutafuta alama sita Ligi ya Mabingwa Afrika, lazima tuhakikishe tunafanya vizuri mechi iliyopo mbele yetu ya ligi, wachezaji wanatakiwa kufikiria kilichopo mbele yetu ambayo Mtibwa Sugar, mchezo huu unatusaidia kujiandaa dhidi ya Medeama FC nyumbani kuvuna alama tatu muhimu” amesema Gamondi

WMA yawaita wenye mashaka kuhakiki upya vipimo
Dullah Mbabe aomba muda kujitafakari