Kocha msaidizi wa Young Africans Cedric Kaze amesema kikosi chake kinaingia katika miezi miwili migumu lakini wamejipanga kupambana kuhakikisha wanafikia malengo ya kushinda mechi zote ili kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ msimu huu.
Kocha huyo amesema mara kadhaa amekuwa akiwasisitiza wachezaji kuongeza umakini na kujifunza mbinu mpya ili kuhakikisha wanafanikiwa katika malengo waliyonayo ya kushinda michezo yote iliyoko mbele yao.
“Hii miezi miwili ya fainali kwetu kwa sababu tunahitaji kupambana kushinda michezo yote iliopo mbele yetu, tunacheza na Azam FC halafu mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ (dhidi ya Geita), kabla ya Simba SC hizo zote ni mechi za muhimu kwenye makombe mawili tofauti,” amesema Kaze.
Amesema kiufundi ni michezo michache lakini ni migumu na iliyo muhimu kupata matokeo chanya wakati msimu huu 2021/22 ukielekea ukingoni.
“Mei ni mwezi wa kumalizia kila kitu, sasa unaweza kuona jinsi ratiba ilivyo na umuhimu, tunahitaji kufanya mazoezi ya pamoja kwa muda mrefu na kupata michezo ya kirafiki, kujiweka sawa katika kufikia malengo yetu,” amesema Kaze.
Ameongeza mchezo dhidi ya Azam FC ni muhimu na unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa lakini dhamira yao ni kuhakikisha wanapata alama tatu.
Kocha huyo kutoka nchini Burundi amesema tayari ameanza kutengeneza mfumo mwingine wa uchezaji ambao utawasaidia wakikutana na mchezo ngumu, au kwenye viwanja vya mikoani ambavyo si rafiki.
“Tumejipanga kuhakikisha timu inakuwa na mifumo mbalimbali ya uchezaji na si kutegemea mfumo mmoja ambao siku ukitakaa, au ukikuta uwanja hauruhusu, au wapinzani kukudhibiti, basi timu inakosa njia nyingine ya kufanya,” amesema Kaze.
Katika hatua nyingine Kocha Kaze ameongeza kuwa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mafunzo FC ya Zanzibar uliochezwa Jumatano iliyopita kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, kuna wakati alichezesha mastraika wawili mbele, Fiston Mayele na Heritier Makambo, wakiwa na mfumo wa 4-4-2, lengo ikiwa ni kutazama mfumo mwingine, hasa pacha ya wachezaji hao wawili mbele, ambao anaamini baadaye unaweza kuwasaidia.
“Tulianza na mfumo tuliozoea, lakini baadaye tukachezesha mastraika wawili mbele, hiyo ni kutaka kujaribu aina nyingine ya mfumo, maana kuna siku tutataka kutumia mastraika wawili, kama siku hiyo mechi itakuwa ngumu, matokeo mazuri hajayapatikana, au kwenye viwanja vigumu, sasa tunaona kama tunaweza kuwatumia Mayele na Makambo wote kwa pamoja ili wakae pale mbele, wawape presha mabeki, mawinga nao wawe wanakwenda pembeni na kupiga krosi nyingi,” Kaze amesema.
Young Africans yenye alama 48, ndio timu pekee mpaka sasa haijapoteza mchezo wowote kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa inaongoza katika msimamo baada ya kushinda michezo 15 na sare michezo mitatu.