Kikosi cha Young Africans leo Ijumaa (Januari 08) kitatupa karata yake ya mwisho kwenye hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2021 inayoendelea kisiwani Unguja, Zanzibar kwa kucheza dhidi ya Namungo FC.
Young Africans iliyo kundi A na timu za Jamhuri na Namungo FC, itahitaji ushindi kwenye mchezo huo, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali, baada ya kuanza kwa matokeo ya sare ya bila kufungana siku ya Jumanne (Januari 05).
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Young Africans, Hassan Bumbuli, amesema kwa muda mrefu sasa hawajalitwaa kombe hilo, msimu huu wamepeleka kikosi kamili ambacho wanaamini kitapambana na hatimaye kufanya kile kinachotarajiwa na mashabiki wa timu hiyo.
Bumbuli amesema mchezaji wao ambaye amekuwa kipenzi cha wanachama na mashabiki wa timu hiyo, Saido Ntibazonkiza huenda akarejea tena uwanjani baada ya kutoonekana katika mechi ya kwanza kwa sababu ya kuwa majeruhi.
“Hatuangalii tulipojikwaa, na kocha ametambua upungufu wa mechi ya kwanza. Huenda leo akamtumia Saido aliyekuwa majeruhi kwa sababu tunahitaji kujiweka pazuri na kutinga hatua ya nusu fainali,” amesema Bumbuli.
Hata hivyo Namungo FC inayonolewa na kocha kutoka Zanzibar Hemed Suleyman Morocco, itahitaji kupambana kwenye mchezo huo, ili kuwa na mwanzo mzuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo wanashiriki kwa mara ya kwanza.
Namungo FC ambayo pia imesonga mbele katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Al Hilal Obeid kwa ushindi wa jumla wa mabao matano kwa matatu, imekua na kiwango kizuri cha kupambana na timu pinzani, tangu ilipoanza kunolewa na kocha Morocco.