Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, leo Ijumaa (Desemba 08) kinatarajiwa kuwasha moto nchini kitakaposhuka dimbani kuvaana na Ghana Medeama katika mchezo wa Mzunguuko watatu wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAFCL).

Young Africans itakuwa ugenini katika mchezo huo utakaochezwa kuanzia saa 1.00 usiku, Uwanja wa Baba Yara Sports uliopo Kumasi nchini Ghana.

Young Africans ilianza Hatua ya Makundi kwa kukubali kichapo cha mabao 3-0 mbele ya CR Belouizdad ya Algeria na ikatoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Kocha wa Young Africans Miguel Gamondi, amesema amekiandaa kikosi chake vizuri kuhakikisha kinapata pointi tatu katika mchezo huo na kujiweka katika nafasi nzuri.

Amesema wanachohitaji ni pointi tatu ambazo zitawasogeza katika nafasi za juu katika msimamo wa Kundi D, ambalo wamepangwa.

“Tunatambua kila timu imejiandaa kupata pointi tatu kuweza kufuzu hatua inayofuata, tumejiandaa vizuri na tunaomba mashabiki wa timu yetu waendelee kutuombea dua na kutusapoti hii inawapa moyo wachezaji wa kupambana zaidi,” amesema.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Rodgers Gumbo, amesema wachezaji wapo tayari kwa mchezo huo wakiamini watapata ushindi.

Amesema viongozi wanaimani na Benchi la Ufundi pamoja na wachezaji wake kwamba wataweza kuwapa pointi tatu mbele ya Medeama SC.

“Tuna imani na wachezaji wetu, watatupatia matokeo ambayo tunayataka, tunaomba kila Mwanayanga aiombee timu yetu tuweze kupata tunachokihitaji,” amesema.

Young Africans inaburuza mkia katika msimamo wa Kundi D ikiwa na pointi moja, wakati Al Ahly ikiwa kinara kwa pointi nne ikifuatiwa na CR Belouizdad na Medeama SC zenye pointi tatu kila moja.

Simba SC yaifanyia ukachero Wydad Casablanca
Twiga Stars yalamba Milioni 200 za Rais Samia