Uongozi wa Klabu ya Young Africans, umeweka wazi kuwa kushindwa kupata ushindi dhidi ya watani zao wa jadi Simba SC ni mwanzo wa kulipa kisasi wakikutana kwenye Ligi Kuu Bara.
Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, Agosti 13, 2023, ilishuhudiwa Young Africans ikivuliwa taji la Ngao ya Jamii na Simba SC waliopata ushindi wa Penati 3-1 kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Akizungumza jijini Dar es salaam Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe, amesema wakikutana kwenye ligi hakuna mshindi anayepatikana kwa Penati kama ilivyokuwa kwenye mchezo uliopita.
“Fainali ni fainali na wachezaji wetu wamecheza fainali kubwa kwenye mashindano ya kimataifa ambayo ilikuwa hatua ya Kombe la Shirikisho Afrika, hivyo uzoefu upo kwa ushindi walioupata tunawapongeza.
“Lakini ninapeda kusema kuwa wachezaji walionesha uwezo mkubwa, tunakwenda kwenye ligi, huku tukikutana hakuna Penati, huo ni uzuri, wanapaswa wasijisahau katika hilo, tupo imara,” amesema Kamwe.
Ikumbukwe kuwa, Kariakoo Dabi ya kwanza kwa msimu wa 2023/24 ndani ya Ligi Kuu Bara, inatarajiwa kuwa Novemba 5-2023 ambapo Simba SC watakuwa wenyeji wa Young Africans kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.