Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umeahidi kumpa pongezi Waziri mpya wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro kwa kutoa kipigo kizito kwa wapinzani wao kutoka Sudan Al Merreikh.

Keshokutwa Jumamosi (Septemba 30) Young Africans itaikabili Al Merreikh ikiwa ni mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika ambao utachezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.

Afisa Habari wa miamba hiyo ya soka nchini Tanzania, Ally Kamwe amesema mbali na kumpongeza Waziri, pia wanataka kuweka historia ya kutinga hatua ya makundi mbele ya kiongozi huyo mpya.

“Tuna zawadi nono kwa Waziri Ndumbaro, sababu tunaamini ni kiongozi shupavu kwenye michezo lakini tunataka kuweka historia kwa kuwa timu ya kwanza Tanzania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika yeye akiwa Waziri wa Michezo,” amesema Kamwe.

Kiongozi huyo amesema wapinzani wao Al Mereikh wanatarajia kuwasili Dar es salaam leo Alhamisi (Septemba 28) wakiwa na msafara wa watu 40.

Amesema maandalizi yote kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri na kwenye kambi yao wachezaji wote wapo fiti kwa ajili ya mchezo huo ambao wamekusudia kuonesha kiwango cha hali ya juu zaidi ya ilivyokuwa mchezo uliopita.

Victor Osimhen kuishtaki SSC Napoli
Alejandro Garnacho amkosha Ten Hag