Katika kuhakikisha wanatimiza malengo ya kutetea Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya kimataifa, uongozi wa Young Africans umesema utaboresha kikosi chao wakati wa dirisha dogo la usajili kulingana na mapendekezo yatakayotolewa na Benchi la Ufundi, imefahamika.

Dirisha dogo la usajili litafunguliwa kuanzia Desemba 16, mwaka huu na litafungwa ifikapo Januari 15, mwakani.

Moja ya idara inayohitaji kuongezwa nguvu ni ya washambuliaji na hilo limetokana na maelekezo ya kocha, Miguel Gamondi kuhitaji makali zaidi katika safu hiyo.

Kwa sasa safu ya ushambuliaji ya Young Africans inaongozwa na Clement Mzize, Kennedy Musonda na Hafiz Konkoni aliyesajiliwa dirisha kubwa ili kuziba nafasi ya Fiston Mayele, kitu ambacho hajaweza kuonyesha makali kama ilivyotarajiwa.

Rais wa Young Africans, Hersi Said, amesema watafanya usajili katika nafasi chache na tayari benchi la ufundi limeshaanza mchakato wa wachezaji wanaowahitaji.

Hersi alisema licha ya kuwapo na kikosi imara lakini bado wanahitaji kuboresha timu kwa sababu wanataka kufanya vizuri zaidi kuliko msimu uliopita.

“Tuna mashindano mengi na muda hautakuwa rafiki lakini tunatarajia kupokea mapendekezo kutoka kwa kocha juu ya nafasi gani anazotaka tufanye usajili.

Mapendekezo yakitufikia, tutaenda kuyafanyia kazi haraka kwa sababu tuna mechi kubwa ikiwamo michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, lazima tuongeze nguvu,” amesema Hersi.

Kuhusu mbio za ubingwa, Hersi amesema ni mapema sana na kushinda mechi dhidi ya Simba SC haina maana njia ya kutwaa taji hilo ipo karibu.

“Ndio kwanza tumecheza michezo tisa, huwezi kudai ubingwa upo karibu, bado ligi inaendelea baada ya mechi yetu jana na Coastal Union kwa mwezi Novemba hatuna mechi nyingine hadi Februari ambapo ligi itaendelea.”

“Hapa kati tutapisha michuano ya AFCON, lakini Desemba tutakuwa na michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Januari tutaenda Mapinduzi, baada ya hapo ligi itaendelea na tutakuwa na mechi mfululizo,” amesema rais huyo wa Young Africans.

Hali ya upatikanaji wa Umeme imeimarika - Kapinga
Sospeter Bajana achekelea rekodi mpya