Klabu ya Young Africans imepanga kusajili wachezaji nyota wapya ili kukiongozea nguvu kikosi chao kinachohitaji kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Jeuri ya usajili ndani ya klabu hiyo imekuja baada ya Shirikisho la Soka la Duniani ‘FIFA’, kuiondolea kifungo cha kufanya usajili, baada ya kumlipa kiungo kutoka nchini Burundi Gael Bigirimana
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema mbali na Mshambuliaji, Ranga Chivaviro, kutoka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, mabingwa hao watetezi wa Ligi KuuTanzania Bara wameanza mazungumzo ya kuwasajili, Benson Mangolo wa Jwaneng Galaxy ya Botswana na Bonaventure Bonito wa Tengueth ya Senegal.
Chanzo hicho kilisema winga wa Power Dynamo ya Zambia, Joshua Mutale, naye yuko katika rada za Young Africans pamoja na mshambuliaji wa Medeama, Jonathan Sowah na Daniel Adjetey, wote raia wa Ghana.
Hata hivyo, Young Africans itapambana na watani zao Simba SC katika kuwania saini za Mangolo na Mutale huku nyota Adjetey akitajwa kutakiwa na Geita Gold FC ya mkoani Geita.
Chanzo hicho kimeongeza Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi, amemtaja Bonito kuwa ndiye mchezaji namba moja anayemhitaji katika kikosi chake kwa ajili ya kumsaidia, Khalid Aucho, ambaye akikosekana ama kwa kutumikia adhabu ya nje au majeruhi, anakosa mbadala sahihi.
“Tangu aondoke Mayele (Fiston), tunahaha upande wa mshambuliaji, Hafiz Konkoni siyo mchezaji mbaya, ila ni kwa sababu aliyeondoka alikuwa na kiwango cha hali ya juu na hiki ndicho kitakacho wahukumu washambuliaji wote watakaotua hapa.
Wanachama na mashabiki wanatataka kuwalinganisha na Mayele. Huenda Sowah wa Medeana na Chivaviro wanaweza kujaribu kuvaa viatu vya Mayele” kimesema chanzo chetu.
Ofisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe, amesema tayari Gamondi ameshawasilisha ripoti yake ya ufundi muda mrefu na imeshaanza kufanyiwa kazi.
Kamwe amesema Young Africans imedhamiria kufanya vizuri zaidi katika msimu huu na ili ifikie malengo yake, inatakia kuimarisha kikosi chake kwa kusajili wachezaji wenye ubora na uzoefu wa kucheza mashindano ya kimataifa.
“Gamondi ameweka wazi ni maeneo gani yanatakiwa kufanyiwa marekebisho, ni aina gani ya wachezaji wanaotakiwa kuja kuiongezea nguvu timu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara, kuna Kombe la FA ambalo halijaanza na Kombe la Mapinduzi.
“Tunataka ikifika mzunguko wa pili, hawa tunaowaongeza wawe wameshapatikana, dirisha likifunguliwa kazi yetu itakuwa ni kutangaza wachezaji na si kutafuta, tumeshazungumza na nyota tunaowahitaji ili dirisha dogo likifika wanajiunga haraka na kikosi kwa sababu hakuna muda wa kusubiri” amesema Kamwe
Wakati huo huo, Young Africans tayari imekamilisha usajili wa kiungo wa JKU FC na Timu ya Taifa ya vijana Zanzibar, Shekhan Ibrahim, kwa kumpa mkataba wa miaka mitatu.
Katibu Mkuu wa JKU, Shadhily Khatib, amesema nyota huyo kwa sasa sio mali yao baada ya kukamilisha taratibu za kujiunga na Young Africans na kinachosubiriwa ni dirisha dogo la usajili kufunguliwa rasmi.
“Ni kweli kwa sasa Shekhan sio mchezaji wetu kwa sababu amesaini mkataba wa miaka mitatu na tumeshamalizana na Young Africans,” amesema Katibu huyo.