Mabingwa wa Soka Tanzania bara Young Africans wametambulisha wachezaji wapya watano hadi sasa ambapo watatu ni wa kigeni na wawili wazawa, lakini imefahamika kuwa klabu hiyo iko mbioni kushusha wengine wanne ili kufunga hesabu.
Beki wa kati Mganda Gift Fred kutoka SC Villa ya Uganda, winga Mkongomani Max Nzengeli kutoka Maniema na beki wa kulia Muivory Coast Kouassi Attohoula Yao kutoka ASEC Mimosas ndio wa kigeni waliotambulishwa huku wazawa ni beki kiraka Nickson Kibabage kutoka Singida Fountain Gate na kiungo Jonas Mkude aliyeachwa Simba SC.
Baada ya hao huenda ikaendelea na usajili na majina manne ambayo yapo hatua za mwisho kumwaga wino ni kama ifuatavyo: Jina la kwanza ni la winga wa kushoto kutoka Marumo Gallants, Muafrika Kusini Mahlatsi Makudubela (33).
Winga huyu ni yule mwembamba aliyeisumbua safu ya ulinzi ya Young Africans kwenye mechi za Nusu Fainali Kombe la Shirikisho msimu uliopita nyumbani na ugenini na mabosi wa timu hiyo wanaamini atakuwa mbadala sahihi wa Benard Morrison.
Staa mwingine ambaye faili lake lipo mezani Young Africans ni la kiungo mkabaji Muivory Coast, Zougrana Mohamed (21) kutoka ASEC Mimosas.
Young Africans inaamini huyu atakwenda kuziba pengo la Yanick Bangala anayesubiri kupewa Thank You’ na huyu ndiye anaweza kupewa jezi namba sita aliyokuwa akiivaa Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyetua Azam FC.
Pia mezani kuna majina ya washambuliaji wengine wawili ambao wanatazamiwa kwenda Young Africans kwa mpigo kuziba pengo la staa wa timu hiyo Fiston Mayele ambaye muda wowote naye atapewa ‘Thank You’ akitajwa kutimkia Pyramids ya Misri iliyomwaga mkwanja mrefu kwake na kwa Young Africans.
Yupo Mkongomani Makabi Lilepo (25), kutoka Al Hilal ya Sudan ambaye Young Africans inamuwinda kwa muda mrefu na inaamini huu ndio wakati sahihi wa kumpata na kuvaa jezi ya Wananchi ambapo mazungumzo baina ya pande zote mbili yanaendelea vizuri.
Mwingine ni Mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2021/2022, George Mpole (30), anayekipiga ES Lupopo ya DR Congo kwa sasa.
Young Africans imeonyesha nia ya kumtaka Mpole kwa mara ya pili na duru hii ni baada ya ligi ya DR Congo kusimama kwasababu ya machafuko yanayoendelea nchini humo hivyo wachezaji akiwemo Mpole kupewa nafasi ya kutafuta timu nyingine ili kulinda viwango vyao.
Mazungumzo baina ya Young Africans na Mpole yanaendelea na kama watakubaliana kila kitu basi staa huyo wa Taifa Stars atakuwa Mwananchi.
Pamoja na hao hadi sasa Young Africans imeachana na wachezaji wake Eric Johora, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Dickson Ambundo, Tuisila Kisinda na Morrison na iko mbioni kuachana na Djuma Shaban, Bangala na Mamadou Doumbia.