Mabingwa wa soka Tanzania Bara, Young Africans wamedhamiria wamesema kuweka rekodi mpya kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Young Africans watacheza na AI Merreikh ya Sudan mchezo wa Mkondo wa Pili wa Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo ambapo kwenye mchezo wa awali uliochezwa Kigali, Rwanda wawakilishi hao wa Tanzania waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Kutokana na ushindi huo, Young Africans sasa watahitaji sare ama ushindi wa aina yoyote kutinga Hatua ya Makundi ya michuano hiyo mikubwa kuliko yote katika ngazi ya klabu Afrika.
Ofisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe amesema wanatambua hawana rekodi nzuri kwenye michuano hiyo na wamedhamiria kuweka rekodi mpya msimu huu.
“Sisi hatuna rekodi nzuri kwenye michuano hii. Mara ya mwisho kuingia hatua ya makundi ilikuwa mwaka 1998.
Hilo halina siasa, lakini safari hii tumedhamiria kufika mbali kwenye michuano hii tukianza na kuingia hatua makundi,” amesema Kamwe na kuongeza:
“Tumesikia kauli za Kocha wa Al-Merreikh akisema Young Africans inaogopeka Afrika. Sisi tuliosoma Cuba tumemuelewa, hawezi kutuchota akili, tutauchukulia mchezo wetu dhidi yao kwa umakini mkubwa.”
Kamwe amesema mchezo huo utakuwa maalumu kwa ajili ya kiungo wao Stephan Aziz Ki, hivyo mashabiki wavae bukta na wabebe funguo kama ishara ya kushangilia siku ya mchezaji huyo.