Baada ya kuambulia matokeo mabaya kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, Miamba ya Soka la Bongo Simba SC na Young Africans inatarajia kurudi dimbani mwishoni mwa wiki juma hili katika michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba SC ilipoteza mchezo wake wa Mzunguuko watatu wa Kundi B, Ligi ya MAbingwa BArani Afrika kwa kukubali kufungwa 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca, huku Young Africans ikiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Medeam SC ya Ghana.
Ijumaa (Desemba 15), Simba SC itakuwa nyumbani Uwanja wa uhuru jijini Dar es salaam kuikabili Kagera Sugar FC, huku YounmgA fricans ikitarajia kuikaribisha Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi, Jumamosi (Desemba 16).
Wakizungumza baada ya kurejea jijini Dar es salaam, Kocha wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi amesema Kikosi chake kimeanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar, huku wakiwa na matarajio ya kufanya vizuri.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema pamoja na timu yake kutofanya vizuri katika michezo ya kimataifa, atahakikisha inapata matokeo mazuri na kujiweka sawa ili kurudi kileleni.
Kwa pande wa Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema pamoja na kuwa na kibarua kizito katika mashindano ya kimataifa, bado kikosi chake kina nafasi ya kufanya vizuri katika michezo ya Ligi Kuu.
Benchikha amesema Pamoja kutowajua vyema wapinzani katika Ligi Kuu Tanzania Bara, atahakikisha anakiongoza kikosi chake kupata matokeo mazuri.
“Tumerudi nyumbani na tumeanza maandalizi ya mchezo wetu ujao wa ligi, nina matumaini kuwa timu itafanya vizuri pamoja na kutokuwa na matokeo mazuri katika michuano ya kimataifa,” amesema kocha huyo kutoka nchini Algeria
Katika msimamo wa Ligi Kuu, Simba ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 19 baada ya kushuka dimbani mara nane, huku Young Africans ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 24 baada ya kushuka dimbani mara tisa.