Uongozi wa Young Africans umeonyesha kuchukizwa na kauli ya klabu hiyo kubebwa na Simba SC kwenye michuano ya Kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Kufanya vizuri kwa Simba SC na kutinga hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kutaisaidia Tanzania kuingiza timu nne kwenye michuano ya Bara hilo msimu ujao wa 2022/23.
Bahati hiyo kwa Tanzania inapingwa vikali na Uongozi wa klabu ya Young Africans ambao unaamini timu yao itashiriki Michuano ya Kimataifa kwa nguzu zake na sio kubebwa na mafanikio ya klabu nyingine.
Akizungumza kwa niaba ya Uongozi wa Young Africans Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo Hassan Bumbuli amesema dhana hiyo iliyojengeka kwa mashabiki wengi wa soka la Bongo sio kweli, kwani klabu yao imejizatiti kushiriki Michuano ya Kimataifa kwa kujibeba yenyewe.
Amesema huenda ikawa na faida kwa Tanzania baada ya Simba SC kutinga Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho, lakini sio kwa Young Africans ambayo ina malengo yake yenyewe ya kulitangaza taifa.
“Kwanza watu wasipotoshwe sana, Msimu huu wa 2021/22 Young Africans ilishiriki Michuano ya Kimataifa kwa jasho letu, hatujabebwa na alama za mtu yoyote, na msimu huu tutapambana na kufikia lengo la kwenda kushiriki Kimataifa kwa jasho letu na nguvu zetu kwa mara nyingine tena”
“Suala hilo halijifichi kwa sababu ukiangalia kwa sasa tunafanya vizuri katika Ligi ya hapa nyumbani na tukichukua Ubingwa tutakwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo suala la kubebwa na timu nyingine sio kweli kabisa.”
“Kama Simba SC ameingia Robo Fainali, tumtakie heri katika hilo, lakini haya mengine yanayosemwa kuhusu kutubeba kwa point alizoziongeza CAF, hayana ukweli na mantiki yoyote kwa Young Africans.” Amesema Bumbuli
Msimu huu 2021/22 katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Tanzania iliwakilishwa na Simba SC na Young Africans, huku Azam FC na Biashara United Mara zikishiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans ilitolewa katika Mzunguuko wa kwanza na klabu ya Rivers United ya Nigeria kwa jumla ya mabao 2-0, huku Azam FC ikitupwa nje na Pyramid FC ya Misri na Biashara United Mara ikitolewa kikanunia, kufuatia kushindwa kusafiri kuelekea nchini Libya kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa pili dhidi ya Al Ahly Tripoli ambayo tayari walikua wameshaichabanga mabao 2-0.
Simba SC imesalia kwenye michuano ya Kimataifa, ikishiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa nyumbani mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana. Mchezo wa Kwanza Simba SC ilishinda ugenini mabao 2-0.
Ushiriki wa timu nne Kimataifa msimu huu 2021/22 kwa Tanzania ulichagizwa na Simba SC baada ya kutinga Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na kuiongezea alama nchi kwenye viwango vya ubora vya CAF upande wa Vilabu.