Baadhi ya wachezaji wa Mabingwa wa Kombe la Mapinduzi 2021 Young Africans wamefichua siri ya kuwadhibiti wapinzani wao Simba SC kwenye mchezo wa fainali uliochezwa jana Jumatano (Januari 13), Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja-Zanzibar.
Katika mchezo huo kikosi cha Young Africans kilionesha uwezo mkubwa wa kupambana ndani ya dakika 90 na kuwanyima nafasi Simba SC kushindwa kupiga shuti hata moja lililolenga lango lao.
Wakizungumza baada ya kutawazwa kuwa mabingwa wa Kombe la Mapinduzi 2021, wachezaji hao walisema walifuata maelekezo ya kocha wao Cedric Kaze ambaye aliwahimiza kucheza pasina kuwaachia nafasi Simba SC, ambao wamekua na sifa ya kumiliki sana mpira.
Beki Abdallah Shaibu Ninja amesema: “Kocha alisema tusimpe mtu nafasi ya kumiliki mpira na tulifanikiwa katika hilo, na ndio maana mwisho wa mchezo tumestahili kuwa mabingwa licha ya changamoto ya mikwaju ya penati.”
“Tulifanya maandalizi ya kutosha na tulikua na ari kubwa ya kupambana ndani ya dakika 90, hatuna budi kumshukuru mungu kwa kufikia lengo la kuwa mabingwa wa Mapinduzi Cup 2021.”
Mlinda Mlango Farook Shikalo: “Umekua mchezo mzuri na wenye ushindani mkubwa, tulipaswa kufikia hapa kwa furaha, sina mengi zaidi ya kumshukuru Mungu.”
“Tumefuata yote tulioelekezwa na kocha Kaze, na kila mmoja wetu alitambua jukumu lake uwanjani na ndio maana hata kwenye penati, nilijua natakiwa kufanya nini.”
Mshambuliaji Saido Ntibazonkiza: “Hamasa kutoka kwa kocha wetu ndio mafanikio ya ushindi huu, kila mmoja wetu alipambana kikamilifu hadi tumefikia hatua hii ya kuwa na furaha ya ubingwa.”
“Kila wakati kocha alituhimiza kucheza bila kuchoka na mimi kama sehemu ya timu nilijitahidi kufikia malengo ya kocha na ya timu kwa ujumla, ‘Alhamdulillah’ tumefanikiwa.
Young Africans inayonolewa na kocha kutoka nchini Burundi Cedric Kaze imetwaa taji la pili la kombe la Mapinduzi katika historia ya michuano hiyo, baada ya kufanya hivyo mwaka 2007.