Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wameipongeza Azam FC kwa uungwana iliouonesha kwenye suala la usajili wa kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’ kwa kufuata taratibu na kumaliza usajili wa mchezaji huyo kwa weledi.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia kukamilika kwa dili la mchezaji huyo kuhamia Azam FC akitokea Young Africans baada ya msuguano wa takribani miezi sita, mchezaji huyo akishinikiza kuvunja mkataba wake kutokana na sababu za kimaslahi na nyinginezo.
Afisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe amesema kuwa Azam FC walifuata chaguo namba tatu la klabu hiyo la kwenda kuzungumz nao, kitu ambacho wamekifanya na kumaliza salama.
“Kama unakumbuka baada ya maamuzi ya kamati (Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF) tukatoa machaguo matatu na mojawapo la klabu inayomuhitaji Fei kuja kuzungumza nasi na Azam ikafanya hivyo.
“Kwahiyo Azam FC wamekuwa waungwa kwa kuja kugonga hodi na kuulizia bei ya Feisal waweze kumnunua, hivyo tunashukuru Azam wamekuja mbele wao wakasema wako tayari, ni jambo la kiungwana na ndivypo mpira ulivyo na klabu tumeimaliza biashara hiyo tukimtakia Fei kila la heri,” amesema Kamwe
Fei ambaye amekabidhiwa jezi namba sita Azam FC aliyokuwa akiitumia alipokuwa Young Africans, anawahama Mabingwa hao wa Tanzania Bara baada ya kudumu nao kwa msimu mitano tangu alipojiunga akitokea JKU ya Zanzibar mwaka 2018.